IMEBADILISHWA: Video hii ya Joseph Mbilinyi akizungumzia Tundu Lissu na uchaguzi ujao ni ya kupotosha

Kwenye video asili, Mbilinyi anasema Tundu Lissu sio mhaini na kuthibitisha kwamba watu wa eneo la Nyasa wanaunga mkono kauli mbiu ya ‘no reform no election’.
Video hii kwenye Facebook inayodai kumuonyesha aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) eneo la Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, akimtaja mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA Tundu Lissu kuwa mhaini IMEBADILISHWA.
“Sugu awa mzalendo CHADEMA waachana na no reform no election,” maandishi yanayoambatana na video hiyo yanasema.

Video hiyo inamuonesha Mbilinyi akihutubia mkutano unaoonekana kuwa wa wanahabari, na asikika akisema, “Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA Mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu ni mhaini. Wanachadema wa kanda ya Nyasa na nchini nzima hatutaki na tunakataa kwa nguvu kabisa no reforms no election. Twende kwenye uchaguzi watu wawachague watu wanaowapenda ifike mahali tukae kama taifa tuwe wazalendo tusitunishiane misuli. Tunayoyatengeneza yakiendelea hili taifa litafika wapi? Sio mpaka tuumizane tuuane wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo tokea Kenya mwaka wa 2007. Nchi itulie tuendelee kufanya kazi tujenge nchi yetu wote (sic) kama watanzania.”
Video hiyo ilishirikishwa tarehe 30 Septemba 2025, wakati kesi ya uhaini dhidi ya Lissu ikiendelea mahakamani. CHADEMA imesisitiza kutoshiriki uchaguzi na kushinikiza msimamo wa “no reforms, no election.”
Uchaguzi mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Je, video hiyo ni halali?
Matokeo ya utafutaji wa picha ya skrini ya video hiyo kupitia Google yaliielekeza PesaCheck kwenye video fupi zilizochapishwa na CHADEMA na Mbilinyi zikionyesha matamshi yaliyo katika video inayochunguzwa.
Video iliyochapishwa na CHADEMA tarehe 20 August 2025 inarekodi sehemu ya kwanza ya hotuba ya Mbilinyi. Tofauti na video iliyobadilishwa, anasema: “Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA Mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu aachiwe bila msharti yote kwani yeye sio mhaini. Wote tunajua hii ni kesi ya kisiasa.”
Sehemu zingine za hotuba hiyo zinapatikana kwenye video hii iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Instagram wa Mbilinyi tarehe 21 Agosti 2025.
Kinyume na madai hayo, Mbilinyi anasema: “Wanachadema wa kanda ya Nyasa na nchini nzima tunasimama na wananchi na msimamo wa no reforms no election kwa sababu tunakataa kwa nguvu kabisa sheria za ovyo za uchaguzi zinazoleta kazia kwa wagombea na wapiga kura na tunadai mabadiliko ya sheria hizi.”
Video inayochunguzwa ilifanyiwa mabadiliko katika sehemu zifuatazo: “Tundu Antiphas Lissu aachiwe bila msharti yote kwani yeye sio mhaini” ilibadilishwa kuwa “Tundu Antiphas Lissu ni mhaini.”
Pia, sehemu Mbilinyi aliyosema “Wanachadema wa kanda ya Nyasa na nchini nzima tunasimama na wananchi na msimamo wa no reforms no election kwa sababu tunakataa kwa nguvu kabisa sheria za ovyo za uchaguzi” ilibadilishwa na kuwa “Wanachadema wa kanda ya Nyasa na nchini nzima hatutaki na tunakataa kwa nguvu kabisa no reforms no election.”
Mabadiliko haya yamevuruga muktadha wa video na kuipa maana tofauti, mbali na kuleta taswira kwamba Mbilinyi ameenda kinyume na chama chake cha CHADEMA pamoja na msimamo wao kuhusu uchaguzi ujao.
Hotuba kamili ya Mbilinyi ilichapishwa hapa na hapa.
Tarehe 2 Oktoba 2025, Mbilinyi alichapisha video asili kwenye akaunti yake ya X (awali Twitter) na kuwasihi Watanzania waipuuze video iliyobadilishwa.
PesaCheck imechunguza video kwenye Facebook inayodai kumuonyesha Joseph Mbilinyi akimtaja Tundu Lissu kuwa mhaini na kugundua kuwa IMEBADILISHWA.
Chapisho hili ni miongoni mwa muendelezo wa makala ya kuangalia ukweli ya PesaCheck kwa ajili ya kubaini maudhui yanayoweza kua habari za uongo katika mtandao wa Facebook na mitandao mingine ya kijamii.
Kwa kushirikiana na Facebook and mitandao mingine ya kijamii kama hii, Mashirika ya kuangalia ukweli kama PesaCheck yanasaidia kubaini ukweli katika maelezo.Tunafanya hivyo kwa kuwapa umma maelezo kwa upana na undani wa machapisho wanayoyaona katika mitandao yao ya kijamii.
Je umekutana na habari unazofikiri ni za uzushi au maelezo ya uongo kwenye mtandao wa Facebook? Hii ndo namna unaweza ukaripoti. Na haya ni maelezo zaidi kuhusu njia ambazo PesaCheck inatumia kuangalia maudhui yenyekuzua maswali.

Chapisho hili la kuangalia ukweli limeandikwa na msahili ukweli wa PesaCheck Rodgers Omondi na kuhaririwa na mhariri mkuu wa nakala wa PesaCheck Mary Mutisya. Makala hii imepitishwa kwa uchapishaji na mhariri mkuu Stephen Ndegwa.

PesaCheck ni mradi wa kwanza Afrika mashariki katika maswala ya kuangalia ukweli juu ya pesa za umma. Kwa pamoja ulianzishwa na Catherine Gicheru na Justin Arenstein, mradi upo chini ya Code for Africa shirika kubwa barani linaloongoza katika nyanja ya teknolojia ya urai na uandishi habari wa data. PesaCheck inafanya kazi kusaidia umma kubaini ukweli katika matangazo ya umma yanahusu namba zinazojenga ulimwengu wetu, kwa msisitizo zaidi katika matangazo ya mapato ya umma yanayosaidia serikali kutekeleza Malengo ya Mpango endelevu ya Dunia (SDG) huduma za kijamii, kama huduma za afya, maendeleo ya vijiji na upatikanaji wa huduma za maji. Pia PesaCheck inaangalia usahihi wa ripoti za vyombo vya habari. Kufahamu zaidi kuhusu mradi, tembeleapesacheck.org.
PesaCheck ni mradi wa Code for Africa, kupitia mpango wake wa innovateAFRICA fund, kwa msaada kutoka Deutsche Welle Akademie, na ushirikiano na muunganiko wa vyombo vya habari vya ndani vya kiafrika pamoja na mashirika mengine ya kiraia.



